Saturday 1 August 2015

MSIMAMO WA MTANDAO WA WANAFUNZI TANZANIA{TSNP] JUU YA KATIBA PENDEKEZWA KUELEKEA KURA YA MAONI






IKUMBUKWA MTANDAO WA WANAFUNZI NCHINI ULIFANYA KONGAMANO KUBWA LA WANAFUNZI NCHINI ILI KUCHAMBUA KATIBA YA MH. JAJI JOSEPH WARIOBA NA KATIBA ILIYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUMU LA KATIBA NA KUONA UTOFAUTI ULIOPO NA TUKAJA NA MSIMAMO WA PAMOJA JUU YA KATIBA PENDEKEZWA.


UNAOMBWA USOME KITABU HIKI KWA KINA ILI UJUE MSIMAMO WA MTANDAO WA WANAFUNZI NCHINI [TSNP} DHIDI YA KATIBA PENDEKEZWA "KATIBA YA CHENGE" YALIYOMO KATIKA KITABU/CONTENT YA KITABU CHA MAADHIMIO YA WANAFUNZI JUU YA KATIBA.


TAMKO LA MTANDAO WA WANAFUNZI TANZANIA JUU YA MCHAKATO WA KUPATA KATIBA MPYA 1.0 HISTORIA YA MCHAKATO WA KUPATA KATIBA MPYA


Tarehe 16 Machi mwaka 1977 ikiwa ni takribani mwezi moja tu tangu kuungana kwa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Julius Nyerere aliteua kamati ya watu 20 chini ya Uenyekiti wa Sheikh Thabit Kombo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa ASP kuandaa Rasimu ya Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya hapo Rais aliitisha mkutano wa Bunge la Katiba kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba kama ilivyopendekezwa na Tume ya Thabit Kombo.


Mapendekezo ya Katiba mpya yalijadiliwa na Bunge lililojigeuza kuwa Bunge la Katiba kwa muda wa saa nne tu na kupitishwa kuwa Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndio inayotumika hadi hivi sasa. Katiba hiyo iliridhia pamoja na mambo mengine, mfumo wa Chama Kimoja chini ya Rais mwenye madaraka makubwa pamoja na muundo wa serikali mbili. Mchakato wa Katiba ya mwaka 1977 haukuwashirikisha wananchi ikizingatiwa kwamba Katiba ni sheria mama ya nchi ambayo inatokana na mapokeo ya mila, desturi, imani, taratibu na utamaduni wa jamii husika kuhusu nchi yao inavyotakiwa kujiongoza (kujitawala) na kwa maana hiyo, lazima itokane na maridhiano, maelewano na makubaliano miongoni mwa wadau wote wa jamii husika. Hii ndiyo maana kuna nchi kama Uingereza ambayo kutokana na makubaliano, hakujawahi kuwa na haja ya hata kuiandika Katiba yao.


Hii ni kwa sababu Katiba yao imesimikwa kwenye misingi iliyokubalika na jamii ya waingereza kutokana na mapokeo yao katika maisha yao ya kila siku katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Lakini baada ya miaka takriban 40 ya utawala wa Katiba iliyoandaliwa kukidhi matakwa ya mfumo wa chama kimoja, na kwa kuzingatia mabadiliko makubwa yaliyotokea katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani na nje ya nchi, imeonekana ni muhimu kwa Tanzania kuandika Katiba mpya. Hivyo kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Nambari 8, Sura ya 83, Rais Jakaya Kikwete aliteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji MstaafuJoseph Warioba na kupewa majukumu ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya aina ya Katiba wanayoitaka, kuandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kuirejesha Rasimu hiyo kwa wananchi ili kujadiliwa kupitia Mabaraza ya Katiba. Baada ya hatua hiyo ilifuata hatua ya kuandaa Rasimu ya Katiba kwa kuzingatia mapendekezo ya wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba. Mnamo Desemba 31, 2013, Tume ya Jaji wa Warioba iliwasilisha Rasimu ya Katiba kwa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar. Kufuatia kukamilika na kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba, Rais Kikwete aliteua wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ambao pamoja na Wabunge wa Bunge la Muungano na wale wa Baraza la Wawakilisha wanakamilisha idadi inayotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 8 na Sura ya 83 Toleo la Mwaka 2013.


 February 18, 2014 Bunge Maalum la Katiba lilianza shughuli zake rasmi mjini Dodoma. Hata hivyo, mwenendo la Bunge Maalum la Katiba, hususani malumbano yasiyokuwa na tija kama vile madai ya posho, ushabiki wa kivyama, tofauti za kiitikadi zisizo na tija, ghiliba pamoja, ubinafsi na jazba miongoni mwa wajumbe, kumeligeuza Bunge hilo kuwa ulingo wa mifarakano badala ya maridhiano, muafaka, maelewano, mashauriano, mshikamano, amani , upendo na uzalendo. Ni kwa sababu hiyo na kwa kuzingatia kuwa vijana ndio taifa la kesho na kwamba ndio watakaoathirika au kufaidika na matokeo ya Katiba mpya, Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (yaani Tanzania Students Network Programme) ukaamua kuandaa Kongamano la siku moja kwa ajili ya wanafunzi wa ngazi mbalimbali kutoka shule, Taasisi na vyuo vya elimu ya juu. Kongamano la wanafunzi lilijumuisha uwakilishi wa Taasisi za elimu zaidi ya 15 na wanafunzi 70 wakiwa wawakilishi wa vyuo vikuu, vya kati na shule za sekondari. Kongamano hili limefanyika katika hoteli ya Landmark, Jijini Dar es Salaam Aprili 16,2014.


2.0 MAMBO YA KUZINGATIA YALIYOMO KATIKA RASIMU YA KATIBA


Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili imesheheni mambo mengi mazuri na endelevu ambayo watanzania wanapaswa kuyapigania badala ya kupelekeshwa kwenye mambo yasiyo na manufaa kwa walio wengi. Kwa kiasi kikubwa Rasimu ya Katiba inapingwa na watu wenye madaraka au wale ambao kwa njia moja au nyingine wataathirika la mabadiriko yanayopendekezwa katika Rasimu ya Katika Mpya. Kongamano la vijana linatoa rai kwa vijana, umma na wajumbe wa Bunge Maalumu la katiba kuzingatia baadhi ya mambo ya msingi kwenye Rasimu kama ifuatavyo:


1. Kupunguzwa kwa madaraka ya Rais na kuondolewa Bungeni pamoja na Mawaziri wake;


2. Kuwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha Wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati wowote (Recall Powers);


3. Kuwepo ukomo wa matumizi na Deni la Taifa;


4. Kuwepo kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakavyogharamia mambo ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka 22 hadi 7;


5. Kuwepo ukomo wa idadi ya mawaziri wasiozidi 15;


6. Kuwepo ukomo wa idadi ya wabunge wasiozidi 75;


7. Kuwepo ukomo wa vipindi kwa wabunge –miaka 15 ya vipindi vitatu vya miaka 5 kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano;


8. Kuwepo kwa Tunu za Taifa (Core Values);


9. Kuwepo kwa Maadili na Miiko kwa viongozi (mathalani kutenganisha biashara na uongozi ili kuepusha mgongano wa maslahi);


10. Kuwepo kifungu cha kuzuia Bunge kubadili baadhi ya masharti mahususi ya Katiba (entrenched provisions) isipokuwa kwa ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni (mathalani Malengo Makuu ya Taifa, Haki za Binadamu)


  11. Kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi;


12. Kuwepo uwiano wa uwalikishi wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume; pamoja na


13. Kuwepo kwa mgombea binafsi.


3.0 MAANDALIZI YA KUELEKEA KURA YA MAONI


Sheria ya Kura ya Maoni imeweka utaratibu utakaotumika kwenye kura ya maoni ikiwemo namna ya kuikubali Katiba Inayopendekezwa.Ili tupate Katiba Mpya inapasa Katiba inayopendekezwa ikubaliwe kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka Tanzania Bara na zaidi ya asimilia 50 kutoka Zanzibar. Jibu la swali litakalotolewa kwa ajili ya Kura ya maoni kwa wapiga kura litakuwa ni NDIYO au HAPANA. Kipindi cha elimu kwa umma kitakachofuatiwa na kampeni kutoka pande kuu mbili ambazo ama zinaunga mkono Katiba inayopendekezwa au zinapinga Katiba inayopendekezwa. Ikumbukwe, Tume ya Uchaguzi ndio imepewa jukumu la kutoa elimu kwa mpiga kura. Kongamano la Wananfunzi linatoa rai kwa vijana kuzingatia yafuatayo:-


1. Kuifahamu historia ya Katiba tangu uhuru;


2. Kufuatilia mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba na kuchambua kinachoongelewa na kuamuliwa;


3. Kuacha kuyumbishwa na misimamo isiyokuwa na tija kwa maslahi mapana ya taifa.


4. Kuwahamasisha vijana wengine hasa wale walioko mitaani ili kuwajengea ufahamu;


5. Kushirika katika zoezi la kuboresha daftari la wapiga kura kwa kujiandikisha; na


6. Kushiriki katika kura ya maoni.


4.0 MAAZIMIO YA KONGAMANO LA VIJANA


Washiriki wa Kongamano walipata muda wa kutafakari kwa kina juu ya Mchakato wa Katiba Mpya na mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba. Washiriki wanapendekeza yafuatayo:-


A: Kuhusu Mchakato wa kupata Katiba Mpya


1. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitumia muda vizuri pamoja na kutoa matokeo mazuri sana;


2. Tume imetimiza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa


3.Tume iliwafikia walengwa;


4.Makundi mengi yalishirikishwa katika kutoa maoni na hivyo kuwa na uwanja mpana kwa kukusanya maoni;


5. Kupuuza kazi nzuri ya Tume na Mapendekezo yake ni hasara kubwa kwa Taifa ukizingatia uwekezaji mkubwa hali na mali kipindi chote cha uhai wake.


6. Vyama vya siasa vimehodhi mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa kuweka maslahi kivyama badala ya maslahi mapana ya wananchi na ya Taifa.


7. Kumekuwa na fununu za vitendo vya rushwa, vitendo hivi kwetu vijana havivumiliki na tunavilaani.


B: Kuhusu mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba


1. Mwenendo wa Bunge Maalumu La Katiba umekosa staha miongoni mwa wajumbe.


2. Wabunge wa Bunge Maalumu La katiba wanayumbishwa kwa sababu wamekwenda Bungeni pasipo maandalizi ya ajenda iliyoko mbele yao.


3. Kuna kila dalili kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanatumika kukidhi matakwa ya wachache au matakwa ya kivyama Kwa kuacha kujadili Rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi kinyume na matakwa ya sheria ya mabadiliko ya katiba ya Mwaka 2011.


4. Bunge Maalumu La Katiba limejaa wanasiasa kutoka vyama vya siasa badala ya makundi ya kijamii na matokeo yake kujadili ajenda za vyama vya siasa badala ya maoni ya wananchi kama ilivyowasilishwa na Tume.


5. Mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba unaangalia zaidi maslahi ya muda mfupi ya kivyama hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 badala ya maslahi ya watanzania kwa ujumla wao;


6. Sehemu ya kwanza ya Bunge Maalum la Katiba limetumika vibaya kwa upande wa muda na rasilimali fedha;


7. Mijadala ndani ya Bunge Maalum la Katika haina tija wala maslahi kwa wengi;


8. Kumekuwepo na upotoshwaji mkubwa wa hoja kwenye mijadala ya vipengele vya Rasimu ya Katiba ndani ya Bunge Maalumu la Katiba;


9. Viongozi wanatumia vibaya madaraka yao


10. Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba watambue kuwa Bunge la Katiba halina mamlaka ya kubadili masharti na mambo ya msingi ya Rasimu ya Katiba, wajibu wao ni kuboresha mambo ya kawaida kwani kilichomo kwenye Rasimu ni maoni ya wananchi.


11. Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba watambue kuwa sisi vijana tutakataa mambo yaliyo nje ya mamlaka waliyopewa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 C: Kuhusu umuhimu wa muafaka, maridhiano na makubaliano kama sehemu ya kufanya maamuzi katika mchakato wa Katiba.


1. Kuna umuhimu wa kuondoa tofauti za kimtazamo na misimamo miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu La Katiba na tunapendekeza kabla ya sehemu ya pili ya Bunge Maalumu La Katiba kurejeshwa kwa maridhiano na maelewano baina ya makundi yaliyotokea sehemu ya kwanza ya Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.


2. Kuna mgawanyiko mkubwa na mfarakano miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kiasi kwamba mwenendo mzima umejaa vitisho na ubaguzi.


3. Majadiliano yalenge kujenga nchi badala ya kuwagawa watu kwa misingi ya rangi, dini, jinsia, itikadi, kabila na eneo;


4. Ni vema yale tu yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ndiyo yazingatiwe kwenye majadiliano kwani ndiyo yaliyowasilishwa na wananchi kwenye Tume, na kama yanapingwa basi msingi wa kuyapinga uwe na sababu za msingi;


5. Muafaka na Maridhiano ufikiwe kwa njia ya majadiliano, maelewano, hoja na kwa amani, kupiga kura kama sehemu ya uamuzi na haki uwe ni uamuzi wa mwisho;


6. Wakati wa majadiliano ni vema kuzingatia maadili na staha badala ya lugha za matusi, kejeli na vijembe na ushabiki;


D: Kuhusu wajibu wa vijana kwenye mchakato wa Katiba


1. Ni muhimu sana kwa vijana kujiandikisha na kisha kupiga kura;


2. Ziandaliwe semina nyingine nje ya Dar es Salaam kwa lengo la kuwafikia wanafunzi wengi zaidi


3.Vijana washiriki katika kusambaza elimu ya mpiga kura kwa njia ya maandishi, ujumbe mfupi na mitandao ya kijamii


4.Vijana tukatae maudhui yaliyotoka nje ya Rasimu ya Tume yasiojengwa katika hoja za kweli na sababu za msingi


5.Vijana wasikubali kurudi nyuma katika kufanikisha mchakato wa Katiba mpya


6.Kuna umuhimu kwa watanzania kujiandaa kuelekea kwenye kura ya maoni, hivyo elimu zaidi itolewe juu ya Rasimu ya Katiba Mpya, ili wananchi waone tofauti ya Rasimu ya Katiba na Katiba itakayopendekezwa.


E: Mapendekezo yetu kwenye Rasimu ya Katiba Wanafunzi, tulichambua Rasimu husika, sura ya kwanza hadi ya mwisho na tukawa na mapendekezo yafuatayo:


           3. SURA YA KWANZA


A] Iongezwe ibara ya kuundwa Tume ya Kusimamia utekelezwaji wa Katiba “Constitutional implementation commission” kwani uzoefu umeonyesha kuwa Katiba inaweza ikatungwa na ikapuuzwa. Mfano, Mahakama ya Katiba haijawahi kuweko tangu mwaka 1964 licha ya kuwemo kwenye Katiba.


B] Ni vema Katiba itamke itikadi ya taifa.Hii itasaidia taifa kutoyumbishwa na tofauti za sera za kivyama. 4.SURA YA TATU MIIKO NA MAADILI YA VIONGOZI A] Sura yote ya tatu,iingizwe kwenye orodha ya mambo ambayo Bunge linakatazwa kufanya mabadiliko ya Katiba isipokuwa kwa njia ya Kura ya maoni. Ibara ya 21 [3] kiongezwe kipengele kidogo kinachosema “kiongozi aliyejiuzuru au kufukuzwa kwa kukiuka miiko na maadili ya uongozi, hataruhusiwa kugombea au kushika nafasi yoyote ya uongozi B] Katika masuala ya elimu, tunapendekeza katika sura ya tatu, sehemu ya kwanza, iongezwe ibara ya 21, itayohusu maadili ya viongozi kusomesha watoto zao ndani ya nchi, kama ishara ya uzalendo wa nchi yao. Ibara hii itasomeka kama ifuatavyo: 21. Kiongozi wa umma, hataruhusiwa kusomesha mtoto/watoto wake nje ya nchi. Atasomesha mtoto/watoto wake ndani ya nchi kama ishara ya uzalendo wa taifa lake. SURA YA NNE A] Ibara ya 31 [1] kiongezwe kipengele cha haki ya kujua na kudai habari B] Afya iongezwe kwenye orodha ya haki za binadamu


C] Makazi yaongezwe kwenye haki za binadamu.


D] Haki za vijana, katika sura ya nne, sehemu ya kwanza, tunapendekeza ibara ya 44, Inayohusu haki na wajibu wa vijana ifafanuliwe, ipambanuliwe na iwe wazi kama ibara zinazohusu haki za watoto “ibara ya 43”, haki za wanawake “ibara ya 47” zilivyopambanuliwa na kufafanuliwa, kinyume na ibara inayohusu haki za vijana ambayo imeweka kwa ujumla.


SURA YA SABA


A] Ibara ya 72,kuhusu madaraka na majukumu ya Rais yapunguzwe Mfano madaraka anayopewa katika vipengele h,j na f ni makubwa mno na kunahatari ya kuyatumia vibaya. Mfano msamaha wa mfungwa [EPA]


B] Ibara ya 73[2]. Kipengele hiki kinalundika madaraka ya uteuzi wa Rais pasipo sababu ya msingi. Nivyema vyeo hivi vikashindaniwa na watumishi wenye sifa badala ya uteuzi wa kisiasa. B] Ibara ya 79 inayohusu sifa za Rais. Tunapendekeza kuwa, Rais asiwe kiongozi wa chama cha siasa kwani yeye ni alama ya taifa.


C] Ibara ya 87 [1] Kinga ya Raisi. Inapendekezwa kuwa Rais aliyemaliza muda wake, aondolewe kinga kama sehemu ya kujenga uadilifu na uwajibikaji anapokuwa madarakani.


SURA YA KUMI.


Mahakama. Ni vyema Katiba ikatenganisha kwa utimilifu madaraka ya Mihimili mikuu mitatu ya Dola, yaani {Serikali, Bunge na Mahakama} ili kuepusha kuingiliana na migongano. Mfano: si sahihi uteuzi wa Jaji Mkuu kuthibitishwa na Mahakama wakati Spika wa Bunge hathibitishwi na Mahakama, Hali kadhalika Rais kuteua wabunge watano miongoni mwa watu wenye ulemavu. Ni vyema wabunge hao wakachaguliwa na walemavu wenyewe


SURA YA KUMI NA MBILI


Ibara 190 [1] Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Inapendekezwa Tume ya Uchaguzi iwe ni taasisi kamili, inayojitegemea kwa kila kitu [fedha, watumishi na rasilimali nyingine] na uongozi wake upatikane kwa kuomba baada ya nafasi kutangazwa, ili kuwashindanisha wenye sifa na weledi. Tume pia isimamie chaguzi zote kabisa,tofauti na sasa ambapo chaguzi zinasimamiwa na TAMISEMI na WAKURUGENZI WA MIJI NA WILAYA. SURA YA KUMI NA TATU Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [PCCB] iongezwe kwenye orodha za taasisi za uwajibikaji zinazotajwa katika Sura ya 13.


SURA YA KUMI NA TANO


Ulinzi na Usalama.


A] Ibara ya 250 [1] wakuu wa nchi washirika, kamwe wasihusike katika kumwagiza kiongozi wa Jeshi la polisi au Idara ya Usalama wa taifa kuchukua hatua ya kulinda au kuimarisha Usalama wa nchi au eneo. Kwa ajili ya kuepusha matumizi mabaya ya vyombo hivi, jukumu hilo libakie kwa kiongozi mmoja tu, yaani Raisi wa shirikisho. B]Inapendekezwa Serikali washirika ziruhusiwe kuunda polisi wasaidizi{auxiliary police} wao kama ilivyo kwa City councils.

No comments:

Post a Comment

Students!!!!!!!!!
For Nation....

Students!!!!!!!!!
Together we have the power.